Historia
Usuli Wetu
Tarehe 13 Juni 2019, Bunge la Tanzania lilipitisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2019 iliyoanza kutumika tarehe 1 Julai 2019. Sheria hiyo iliifanyia marekebisho Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura ya. 438 iliyorekebiwa mwaka 2019 ili kuanzisha ofisi inayojulikana kama “Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi - Tax Ombudsman Service Tanzania”.
Ofisi ilikusudiwa kulinda haki za walipa kodi dhidi ya matumizi mabaya ya mamlaka ya maofisa wa kodi na kuhakikisha uwazi, ufanisi na usimamizi mzuri wa kodi nchini Tanzania. Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi ni chombo huru chenye jukumu la kupitia na kushughulikia malalamiko yote ya walipakodi kuhusu huduma, masuala ya kiutaratibu na kiutawala yanayoweza kujitokeza katika usimamizi wa sheria za kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamishna Mkuu au wafanyakazi wa TRA.
Ili kutekeleza kazi hii, tarehe 4 Machi 2022 Waziri wa Fedha alitunga Kanuni za Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi chini ya Tangazo la Serikali Na. 105 la 2022 ("Kanuni za Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi") ambazo zinatoa masharti ya usimamizi wa Ofisi, uteuzi wa wafanyakazi wake na kanuni zitakazozingatiwa na Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, na Kanuni za Usimamizi wa Kodi (Taratibu za Malalamiko na Taarifa za Kodi) chini ya Tangazo la Serikali Na. 106 la 2022 ("Kanuni zaUtaratibu wa Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi") ambazo zinaeleza utaratibu huo wa kuwasilisha malalamiko kwa Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, na kuendesha na kushughulikia malalamiko na Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi.